Thursday, December 1, 2016



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI;

Imetolewa na Afisa mawasiliano na Uchaguzi –CUF TAIFA, 29 Novemba 2016.

"DHAMBI YA USALITI INAMTESA LIPUMBA".

Jana tarehe 28/11/2016 Lipumba alizungumza na waandishi wa habari kwa kile alichokiita kujibu hoja za Katibu Mkuu wa Chama Maalim Seif Sharif Hamad alizotoa katika mkutano na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi.
Tunasikitika kusema kuwa Lipumba ameshindwa kujibu hoja na badala yake amejikita kwenye majigambo na kujifaharisha na waganga wa kienyeji na vyombo vya dola kuwa wamemuhakikishia ataendelea kuwa Mwenyekiti wa CUF mpaka mwaka 2019.

Kwanza tunawashukuru watanzania kwa kuendelea kumpuuza kwani yapo masuala mengi yanayowasumbua watanzania kama kuyumba kwa uchumi na serikali ya awamu ya tano ambayo Lipumba alijenga ubia nayo tangu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana ikiwa ni pamoja na mwendelezo wa urafiki wa kuihujumu CUF.

Ndiyo maana hivi sasa anashindwa kufungua mdomo wake kukosoa na kushauri hadhara njia mbadala za kuondokana na hali hii badala yake anampongeza Mheshimiwa Rais Magufuli na serikali yake kwa kuharibu uchumi wa nchi. Lipumba huyu siyo yule tuliyekuwa tunamfahamu. Na haya ndiyo madhara na gharama ya kuwa kibaraka wa mfumo kandamizi wa demokrasia.

Ameshindwa kujibu hoja na ameshindwa kukanusha juu ya uhusiano wake na Jeshi la polisi nchini ambao umekuwa ngazi ya kuhujumu Chama huku vitendo vya kihalifu vya Lipumba na wapambe ake vikikingiwa kifua. Amejitwika jukumu la kuwa msemaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na kushindwa kupinga hoja ya jaribio la kutaka kuiba fedha za ruzuku za Chama kwa kutaka kufungua akaunti binafsi akishirikiana na Jaji Francis Mutungi. Ameshindwa kujibu hoja kuwa wapambe na wahuni wake wanafanya uhalifu na kulindwa na Polisi na bila kuchukuliwa hatua zozote. Lakini pia hajawaambia Watanzania sababu za kujiuzulu kwake na sababu za kutaka kulazimisha tena kuendelea kuwa Mwenyekiti wa The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi).

Lipumba anajidhalilisha na kujivunjia heshima na mwenye njaa ya ruzuku ni yeye aliyetaka kufungua akaunti yenye jina la chama ili ajichukulie fedha za chama kinyume na taratibu na hali akijua hana mamlaka ya kufanya hivyo.

Hata kama angekuwa ni ‘Mwenyekiti Halali wa Chama’ kwa mujibu wa Katiba ya CUF; Majukumu ya Mwenyekiti wa Chama Taifa yamebainishwa katika ukurasa wa 82 Ibara ya 91(1)(a-m) ambayo hayampi mamlaka ya kufanya haya anayoyafanya Lipumba ikiwemo kutaka kudhibiti fedha na mali za Chama.

Katiba ya CUF ambayo yeye anadai na kusisitiza kutaka ifuatwe kwa kuiangalia zaidi Ibara ya 117(2) pekee, imempa Majukumu muhimu Katibu Mkuu wa Chama katika ukurasa wa 85 Ibara ya 93(1)(a-k)(2) kuwa;
a) “Atakuwa Mtendaji Mkuu wa Chama na pia mwajibikaji mkuu wa shughuli zote za utendaji za Chama kitaifa” Ibara ya 93(1)(a).

b) "Atakuwa na dhamana ya ofisi za Makao Makuu na Ofisi Kuu ya Chama” Ibara ya 93(1),(f)

c) "Atakuwa mwajibikaji mkuu wa mambo yote ya fedha na mali za Chama katika ngazi ya Taifa (Chief Accounting Officer)” Ibara ya 93(1),(i).

Kwa hiyo, kitendo cha Katibu Maalim Seif, kuhoji juu ya UHUNI wa Jaji Mutungi wa kuzuia RUZUKU ya CUF kwa sababu Mutungi aliona haitamfikia Lipumba ili kutumika kwa malengo ya dola kuisambaratisha CUF, ni kitendo muhimu sana kikatiba, ni kitendo kinachodhihirisha kuwa Katibu Mkuu anatimiza wajibu wake kama Msimamizi Mkuu wa masuala ya fedha za chama. Kama ni njaa anayo BWANA YULE, ambaye alipokwenda Lindi na Mtwara alibeba vimemo na kuingia benki ya NMB tawi hatulitaji na kupewa Tzs 20,000,000 kwa maelekezo ya kada na kiongozi maarufu wa CCM. Wafanyakazi wa Tawi hilo la NMB hadi leo hawaamini inakuwaje kiongozi wa Upinzani aliyejitambulisha kama anayepambana na CCM, kupewa mamilioni ya pesa na viongozi wa CCM.

Njaa! Kama kuna mwanasiasa ana njaa na ametumia maisha yake kutumika ni Lipumba. Lipumba na wahuni wake wakumbushwe juu ya hotuba zake mwaka 2011 baada ya Kikwete kushinda ushindi mwembamba. Lipumba hajawajibu watanzania alikuwa na maana gani kusema "aliokoa jahazi ili Kikwete ashinde uchaguzi" ilihali Lipumba alikuwa mgombea wa CUF. Je,ni kikao gani cha CUF kilimtuma Lipumba akaokoe jahazi na kumpa ushindi Kikwete mwaka 2010?

Lipumba amepoteza weledi wake wa mambo tuliokuwa tunaujua hapo kabla, anazungumza mambo bila Takwimu, bila ushahidi. CUF kama taasisi makini, taasisi Imara imeshafanya maamuzi kupitia vikao halali vya Chama Mkutano Mkuu Taifa na Baraza Kuu la Uongozi Taifa, Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad hana mamlaka ya kuzungumza na Lipumba na kulipatia ufumbuzi suala hili kwa kuwa si lake ni la Chama na Chama kilishafanya maamuzi ya kumvua uanachama. Kazi aliyojipa kwa kupewa bahshishi na washirika wake ya kuvuruga upinzani haitafanikiwa kwa sababu CUF na vyama washirika itaendeleza ushirikiano na kuondoa mapungufu yote yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita ili tuwe na nguvu madhubuti ya pamoja kukabiliana na CCM katika chaguzi zijazo. Kamwe hataweza kuturudisha nyuma na kutuyumbisha.

Lipumba anazungumzia ujumbe wa Maalimu Seif kupitia barua pepe yake ya Disemba 30, 2015 eti kuwa anamtambua! Hii inatia shida kidogo kumuelewa Lipumba, alisema ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida na kadi yake amelipia mpaka mwa 2020, sasa kutumiwa ujumbe ndio imemaanisha kuwa yeye ni ‘Mwenyekiti Halali’ na inadhihirisha kuwa Maalim Seif hana ugomvi binafsi yeye. Inastaajabisha sana kuona kuwa aliyekuwa kiongozi wa kupinga propaganda za CCM leo anatumia propaganda hizohizo dhidi ya Chama cha CUF kutaka kuwabagua watanzania kwa misingi ya udini, ukanda, utanganyika na uzanzibari.

Wakati Maalim Seif anajenga hoja za matukio takribani tisa yaliyotokea katika kipindi cha baina ya Mwezi Agosti-Novemba, 2016 ikiwemo jaribio la utekaji na Jeshi la Polisi kushindwa kutekeleza wajibu wake, yeye amejitokeza kuwa msemaji pia wa jeshi la Polisi, kwa kweli inasikitisha sana. Lipumba aache kuwa na uchu wa madaraka zama zake zimekwisha ndani ya CUF, kutamani kwake kugombea nafasi ya Urais mwaka jana kuliathiriwa na hali halisi ya mazingira na haja ya wakati ule na hayakuruhusu kabisa kwake kuwa mgombea na kufanya vizuri. Eti Lipumba haoni mchango wa Mhe. Edward Lowassa katika UKAWA! Je? Dhamira na nafsi yake zimeacha kumsuta? Mhe. Edward Lowassa amepata asilimia 39 ya kura, Lipumba anakataa kuwa Lowassa hana mchango kwenye mabadiliko ya demokrasia nchini? Lipumba alizoea kupata asilimia 7 ya kura na alijenga ufalme akidhani kuwa ataendelea kuwapiga mnada watanzania na kuchukua hela ili "kuokoa ahazi" kila chaguzi utakapofika?

Kwa upande wa Zanzibar CUF tumeshinda nafasi ya Urais na kushuhudia CCM na Dola wakipora ushindi huo kwa kumtumia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar –ZEC. Lipumba anakataa? Anaunga mkono maamuzi ya mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC? Lipumba anachukia ikielezwa kuwa Mhe. Edward Lowassa amemshinda Magufuli katika matokeo ya kura za Urais Zanzibar!

Kushirikiana na vyama vingine vya siasa ni maamuzi yanayotokana na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambalo bado linatambua uwepo wa ushirikiano wa vyama–UKAWA. Je yeye binafsi kama angekuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa anao uwezo wa kuiondoa CUF katika UKAWA bila kutumia njia za vikao? Mashirikiano haya yanaendelea katika uundaji wa Halmashauri na CUF kuwa na Mameya na Manaibu Meya Je kwa akili ya Lipumba Mameya na Manaibu Meya hawa wajiuzuru ili wasishirikiane na CHADEMA? Aleze sababu za kulazimisha kutaka kuwa mwenyekiti ni zipi wakati alijiuzuru kwa matashi yake binafsi mbali na kuombwa asifanye hivyo? Iweje viongozi wa Dini na wa Chama waliomuomba sana wakati ule asijiuzulu akawakatalia katakata na kuendelea na dhamira yake na hatimaye akakimbia vita na kukiacha chama katika kipindi kigumu cha maandalizi ya uchaguzi mkuu, ilhali leo anadai amezingatia maombi ya viongozi wa dini wale aliowakatalia mwanzo? anadai kuwa alimuandikia barua Katibu Mkuu akajibiwa kuwa asubiri, kwani kwa akili ya Lipumba, kurudi kwake kwenye nafasi ya Uenyekiti wa Chama kwa mujibu wa katiba ya CUF yanafanywa na Katibu Mkuu wa Chama? Huu ni umbumbumbu wa sheria na Katiba ya CUF wa hali ya juu.

Kwa mashirikiano ya CUF na vyama vingine tumeweza kufanya kampeni za uhakika na za kisasa zilizoleta ushindani mkubwa na kuifanya CUF ipate wabunge katika majimbo kumi (10) ya Tanzania Bara na kuongoza Halmashauri nne (4) nchini. Lipumba anakataa na kupinga kuwa hatukupata wabunge 10? Je, anakumbuka kuwa miaka yake 19 ya Uenyekiti wa CUF chama hakikuwahi kuwa na wabunge hata watatu? Leo CUF ina halmashari 4 na madiwani zaidi ya 300, miaka 19 ya Uenyekiti wa Lipumba ndani ya CUF iliwahi kuleta hata halmashauri moja?

Lipumba ametakiwa aeleze sababu za kujiuzuru kwake ni zipi? lakini ameshindwa kufanya hivyo. Lipumba anazeeka vibaya na amekuwa msahaulifu, anapozungumza katika vikao vyake vya ndani maeneo mbalimbali anasema Wazanzibar hawamtaki na kwamba wanataka kujitoa katika makucha ya Wazanzibari, anazungumzia Utanganyika na Uzanzibari, na wapambe wake wanalishikilia bango suala hili. Aache kueneza na kupandikiza chuki kwani ajenda hizo ndizo zimefanya miaka yake 19 ya uongozi ndani ya CUF kukosa lolote la kujivunia.

KUHUSU SUALA LA UMOJA WA KATIBA YA WANANCHI-(UKAWA):

Lipumba ameulizwa na kushindwa kujibu, nani aliyeleta UKAWA ndani ya CUF? Nani aliyeweka saini za makubaliano ya UKAWA pale Jangwani? UKAWA umeanzia Bunge la Katiba. Katibu Mkuu Maalim Seif hakuwa mjumbe wa Bunge la Katiba. Yeye Lipumba ndiye aliyekwenda kumuona Mheshimiwa Lowassa na kumtaka ikiwa CCM itamuengua ajiunge na UKAWA. Akashauri ajiunge na NCCR–Mageuzi na CHADEMA na CUF tumuunge mkono. Ni yeye aliyemtambulisha Lowassa kwa waandishi wa Habari. Lipumba anajaribu kuiweka CUF sokoni, ili iinunue na itumiwe kuudhoofisha upinzani.

Lipumba amezoea na ameshaonja radha ya kutumika, alitumika mwaka 2010 akamsaidia Kikwete kushinda urais, mwaka 2015 alipoona hawezi kugombea urais akajua wanunuzi wataona hana thamani, akaona njia ni kujitoa kwenye chama ili wanachama wavurugike, mpango wake ukafeli vibaya kwani CUF ni taasisi. Wanunuzi wake, CCM, waanze kutafuta bidhaa nyingine kwa sababu CUF ilishamalizana naye. Waendelee kumpa ulinzi wa defender’ za Polisi, wampigie Saluti, wampe uenyekiti wa chama kwa nguvu ya dola n.k. Yote hayo hayataihamisha CUF kwenye ajenda zake katika kuwapigania Watanzania na Wazanzibari kwa ujumla.
Na mwisho sote tunaweza kuendelea kujiuliza swali la msingi, ni mahali gani Duniani kiongozi wa juu wa taasisi kubwa kama CUF ambaye aliwahi kuandika barua ya kujiuzulu na kuiacha ofisi yake kwa muda wa miezi kumi, taasisi ikachagua au kuteua kiongozi mbadala wa nafasi hiyo kisha baadae mtu huyo akalazimisha kurejea katika nafasi yake?

Mwisho:

Tunamtaka Lipumba ajiheshimu na kuacha kujidhalilisha kwa kulazimisha mambo ambayo hayawezekani na yaliyo kinyume na matakwa ya Katiba ya CUF. Chama chako kikishakukataa ndani ya chama, hata kama ungekuwa,na majeshi kutoka mwezini, huwezi kuwa kiongozi wa chama hicho. Tunamtahadhalisha Lipumba na wahuni wake kuwa watabeba Msalaba wa gharama zote zitakazotokana na uharibifu wowote wa mali za Chama utakaojitokeza. Yeye si wa kwanza kujaribu kutumika kutaka kuvuruga CUF na au vyama vya upinzani nchini lakini wote waliotumika muda wa kutumika ulipokwisha walitelekezwa na kufedheheka. Lipumba ashughulikie masuala yanayohusiana na fani yake ya uchumi kama alivyoaihidi wakati anajiuzuru, siasa imemshinda.

CUF imevuka vigingi vingi vizito katika nyakati tofauti kila ilipojaribiwa ikiwa kwa uadui wa ndani au wa nje, mwisho wa vitimbi vyote hivyo, CUF iliibuka mshindi. Tunatoa wito kwa wanachama, wapenzi wa CUF, na watanzania wote kwa ujumla waendelee kuwa na Subira. Hakika CUF ni taasisi makini na imara ya kisiasa nchini, na mwisho wa hili CUF ndiyo itakayoshinda.

"HAKI SAWA KWA WOTE"

No comments:

Post a Comment