Thursday, December 1, 2016


UFAFANUZI WA KAULI YA PAUL MAKONDA.

Na:Goodluck Abel 
"Msinijaribu, ardhi kinondoni nitawashughulikia, hadi mtajuta kuzaliwa. 'Mimi nikisimama hapa, amesimama Mungu', sikuletwa hapa kwa bahati mbaya, nitawatia ndani wote, na hakuna mtetezi wenu, wewe mama unanisikia? hauna wa kukutetea.."

Kauli hiyo imetolewa na kijana wa UVCCM aliyeteuliwa na Rais Magufuli kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ili kuwakomesha wapinzani, Ndg. Paul Makonda.

Ili kuelewa, ni vema kutafakari neno kwa neno, kama ifuatavyo;

1. "Mtajuta kuzaliwa", kujuta kuzaliwa ni hatua ya mwisho ambayo binadamu huifikia hata akamuuliza muumba wake ni kwanini alimuumba, hivyo Makonda anajivika cheo cha muumbaji.

2. " Hakuna wa kuwatetea", kwamba akiamuru yeye, maamuzi yake ni ya mwisho. Lakini katiba na sheria za nchi zinamruhusu mtu kujieleza (natural Justice), na kuwa na utetezi dhidi ya mashitaka yake mahakamani, hivyo: kwa amri ya Makonda, akikuweka ndani unaweza kuozea huko na hakuna wa kukutetea.

3. "Nitawashughulikia", maana yake atatoa adhabu, ambapo katiba ya nchi inasema kuwa mtu hatoadhibiwa kwa kosa lolote, hata la jinai, mpaka itakapothibitika mahakamani kuwa ana kosa, hivyo: Makonda ndiyo mwenye mamlaka na maamuzi ya mwisho juu ya hukumu ya mtu na sio mahakama tena.

4. " Mimi nikisimama hapa, amesimama Mungu", #Astaghfirullah... Yaani Makonda sasa anachukua nafasi ya Mungu, kwa hili nashindwa kufafanua zaidi, naishia kutamka tena 'Astaghfirullah' yaani 'Mungu asamehe'.

5. "Sikuletwa hapa kwa bahati mbaya", hili: kwa bahati mbaya hatufahmu kuna nini nyuma ya pazia hata yeye mwenyewe kukiri kuwa hakuletwa kwa bahati mbaya, maana yake lipo kusudi, na matokeo ya kusudi hilo ni hayo yaonekanayo, mbali na aliyemteua kusema kuwa "nimekuongeza cheo ili kuwakomesha wapinzani wako"

Hapa ndipo tulipofikia mtanzania mwenzangu, tufahamu kuwa nchi yetu ikiupoteza utawala bora unaozingatia sheria za nchi na katiba yetu wenyewe, nchi itatumbukia pabaya siku za usoni.

No comments:

Post a Comment