Kuhusu kesi ya Lema
Anaandika #Wakili Msomi Peter KibatalaTulikubaliana Mawakili wenzangu wa case ya Godbless Lema kuto-post chochote kuhusu case ya Lema mpaka siku Lema anatoka remand; lakini baada ya kuona upotoshwaji na sintofahamu unaofanyika/iliyotokea mitandaoni kuhusu case hii, tumeona ni vyema tukatoa ufafanuzi.
Kama tulivyosema awali; Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimpatia dhamana Lema mnamo tarehe 11 November. Mara baada ya Mahakama kutoa dhamana, Serikali ikatoa taarifa ya kusudio la kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo. Tafsiri yao ya sheria husika ni kwamba baada ya taarifa hiyo ya kusudio hilo, Mahakama haina mamlaka ya kuendelea kuweka masharti ya dhamana mpaka rufaa ya serikali itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Mahakama ikakubaliana na hoja hiyo na kukata kuweka masharti ya dhamana.
Sisi hatukuridhishwa, na tukaandika barua kwa Judge Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ili Mahakama Kuu iitishe Majalada ya case husika na kujiridisha na uhalali wa uamuzi huo. Tulikuwa na sababu za kisheria za hatua hiyo, ikiwemo maoni yetu kwamba uamuzi ule ulikuwa ni mdogo (interlocutory) na hauwezi kukatiwa rufaa au kuombewa marejeo. Mahakama Kuu kwa mamlaka yake ya usimamizi wa Mahakama za chini yake ikatuita kuelezea tatizo.
Kwa bahati mbaya serikali ikawasilisha mapingamizi wakisema tulipaswa kukata rufaa badala ya kuomba Mahakama Kuu iingilie kati kwa mamlaka yake ya usimamizi. Sisi tukasisitiza mamlaka ya usimamizi wa Mahakama Kuu ni kubwa kuliko haki ya kukata rufaa.
Mahakama Kuu mnamo 22/11/2016 ikaelekeza tukate rufaa pamoja na kwamba tayari ilishatuita yenyewe.
Iwe iwavyo, tukapeleka Mahakamani notisi ya kusudio la kukata rufaa. Tukapeleka pia hati ya rufaa.
Leo asubuhi wakati tukijiandaa na usikilizwaji wa Rufaa, serikali ikaleta pingamizi kwamba hatujakidhi takwa la kutoa notisi kabla ya rufaa. Pingamizi lazima lisikilizwe kwanza kwa mujibu wa sheria; vyovyote litakavyomriwa na Mahakama.
Mahakama imeelekeza serikali kuwasilisha hoja zake za maandishi mpaka tarehe 30 November saa 2 asubuhi. Sisi tutajibu siku hiyo hiyo saa 6 mchana, serikali itajibu tena saa 9 alasiri ya siku hiyo hiyo ili uamuzi utolewe tarehe 2 December saa 3 asubuhi. Kisha kutegemea na uamuzi, tutasikiliza rufaa yetu.
Kama tulivyosema awali; michakato ya kisheria huwa haina njia ya mkato. Kwa mfano, mtu akileta pingamizi hakuna namna zaidi ya kulisikiliza kabla ya case/ maombi ya msingi.
Bahati mbaya kuna upotoshwaji unaotokana na baadhi kutaofahamu hasa nini kinatokea mahakamani; kwa mfano, taarifa kwamba leo (28/11/2016) ilikuwa Lema apewe dhamana SI SAHIHI. Leo ilikuwa tusikilizwe rufaa yetu ili kama ilikubalika, Mahakama Kuu iamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi au yenyewe itoe dhamana kwa Lema.
Kwa hiyo: tutajadili pingamizi la Serikali na kutegemea na maamuzi ya Mahakama Kuu hapo Ijumaa 2/12/2016, tutasikiliza rufaa ya Lema. Mahakama Kuu inajitahidi sana kushughulikia suala hili kwa haraka kama tulivyoomba kwa hati ya uharaka.
Lema yuko imara kwa kuwa, tofauti na baadhi yetu, anafahamu 100% nini kinaendelea. Anafahamu sacrifices tunazozifanya kwa niaba yake ili hatimaye apate dhamana.
Ametuagiza kusimama imara bila kutetereka kwa kuwa ametuchagua sisi tumpiganie.
No comments:
Post a Comment